Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi leo alikuwa Mgeni rasmi katika kuwaunga mkono Vijana wa Kikundi cha Sarakasi cha Bungi Muembe Kiwete Wilaya ya Kati kwenye sherehe yao ya kutimia mwaka Mmoja tokea kusajiliwa rasmi.

Sherehe ya Kikundi hicho kiitwacho We are Strong Acrobatic Show ilifanyika katika uwanja wa michezo wa Bungi na kushirikisha pia baadhi ya Vikundi vya sarakasi vya Mkoa wa Kusini Unguja.

Balozi Seif akiwa na baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Kati pamoja na Wananchi wa maeneo jirani ya Kijiji hicho walishuhudia burdani safi iliyoanikiza kwenye uwanja huo na kujumuisha Vikundi vya Sarakasi vya Muongoni, Bihole Bungi pamoja na wenyeji hao We are Strong Acrobatic Show.

Akizungumza na wanamichezo hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwakumbusha Wanamichezo hao kuwa makini katika kuimarisha hali ya amani iliyopo kwa lengo la kuendelea kuwa na fursa nzuri ya kufanya mazoezi kwa utulivu.

Alisema Vijana wa Sarakasi wanahitaji kuungwa mkono na washirika wa michezo pamoja na Serikali Kuu, na hili litawezekana iwapo hali ya amani itaendelea kudumishwa na kila mwananchi wa Taifa hili.

Balozi Seif aliwapongeza Vijana wa Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja kwa jitihada wanazochukuwa za kuimarisha michezo ambayo kwa hivi sasa imekuwa sehemu ya ajira hasa kwa vijana.

Katika kuunga mkono vijana hao wa Sarakasi Balozi Seif aliahidi kutafuta fursa za kuwapatia vifaa vya Michezo yao pamoja na nafasi za Taaluma nje ya Nchi kwa kuimarisha ujuzi walionao.

Mapema akisoma Risala Katibu wa CCM wa Tawi la Bungi Safia Ali Vuai alisema Kikundi hicho cha sarakasi ambacho kiko chini ya Tawi hilo kilianzishwa mwaka 2011 kikiwa na Vijana 30 ambapo kwa sasa wameongezeka na kufikia 50.

Safia alisema licha ya baadhi ya changamoto zinazokikumba kikundi hicho ikiwemo ukosefu wa kiwanja cha mazoezi na vifaa lakini kimepata mafanikio makubwa ya ongezeko la wanafunzi wa sarakasi pamoja kuunda urafiki na baadhi ya vikundi vya fani hiyo Zanzibar na Dara es salaam.

Balozi Seif pia aliahidi kuvipatia vikundi hivyo mchango wa fedha taslim kutokana na juhudi zao wanazochukuwa za kuhamasisha katika mikutano na shughuli za Chama cha Mapinduzi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top