Na: Hassan Hamad,OMKR

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewashukuru wanachama wa chama hicho katika Wilaya ya Kaskazini ‘B’ kwa kujitokeza kwa wingi na kuwa wastahamilivu kwenye mkutano wa hadhara wa CUF jimbo la Kitope, licha ya kuwepo kwa mvua kubwa.

Amesema kitendo hicho kinadhihirisha jinsi wanachama wa eneo hilo walivyokubali na kuamua kukiunga mkono chama hicho.

Akihutubia mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika eneo la Kilombero jimbo la Kitope, Maalim Seif amesema chama hicho kimekuwa kikipigania maslahi ya Zanzibar, ili iweze kujikwamua kisiasa na kiuchumi.

Amefahamisha kuwa katika jitihada za kuwakwamua wananchi kiuchumi chama hicho kinakusudia kutekeleza kwa vitendo sera ya bandari huru, jambo ambalo litaongeza ajira kwa vijana na hatimaye kunyanyua kipato cha wananchi.

Sambamba na hilo, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema lengo la chama hicho ni kuhakikisha kuwa kinajenga mazingira na miundombinu imara ili kuvutia wawekezaji katika sekta mbali mbali zikiwemo utalii na uvuvi wa bahari kuu.

Katika hatua nyengine Katibu Mkuu huyo wa CUF ameelezea kutoridhishwa na kitendo cha jeshi la polisi nchini kuweka vikwazo vya kuwazuia wananchi kutoka maeneo mengine kushiriki kwenye mikutano ya hadhara ya chama hicho.

Amesema CUF hakikushiriki katika kikao baina ya jeshi la polisi na vyama vya siasa kilichofikia maamuzi hayo kutokana na kuweko kwenye mkutano muhimu wa ndani wa chama hicho, na kwamba tamko hilo la jeshi la polisi linakwenda kinyume na Katiba ya nchi.

Amelitaka jeshi la polisi kutoa ufafanuzi juu ya sheria waliyotumia hadi kufikia kutoa tamko hilo ambalo amesema linazuia uhuru wa watu kushiriki shughuli za kisiasa.

Aidha amelishauri jeshi hilo kuzingatia hali ya uchumi na mazingira ya Zanzibar, kwani kitendo cha kuweka vizuizi barabarani kinaleta taswira mbana kwa wageni na kinaweza kuathiri hali ya uchumi, ikizingatiwa kuwa Zanzibar inategemea zaidi sekta ya utalii.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema chama hicho kinapinga kunyimwa uhuru wao wa kikatiba wa kuwazuia wananchi kushiriki katika mikutano ya hadhara kutoka Wilaya moja kwenda nyengine.

Katika risala ya wanachama wa CUF jimbo la Kitope iliyosomwa na bi. Fatma Seif Said, wamesema wameamua kukiunga mkono chama hicho kutokana na mwelekeo wake wa kutaka kuleta ukombozi wa kweli kwa wazanzibari.

Aidha wameomba kujengewa tawi la kisasa katika eneo la Kilombero, ili iwe kielelezo cha kukubalika kwa chama hicho katika eneo hilo.

Katika mkutano huo, jumla ya wanachama wapya 285 wamejiunga na chama hicho kutoka jimbo la Kitope.

0 comments:

 
Top