Na: Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amezindua vikundi saba vya mazoezi katika Jimbo la Gando, na kutoa wito kwa wananchi kufanya mazoezi.

Katika uzindui huo uliofanyika Skuli ya Kizimbani Wete Pemba, Maalim Seif amesisitiza kuwa mazoezi ni muhimu katika kujenga afya za wananchi pamoja na kuimarisha umoja na mshimano miongoni mwao.

Amewahamasisha wananchi kujijenga katika kufanya mazoezi, kwani ni kinga ya maradhi mbali mbali, jambo ambalo linaweza kupunguza gharama za matibabu.

Amesema mazoezi pia yanaibua vipaji vya wanamichezo, na kuahidi kuwa serikali inaendelea kushirikiana na vikundi vya mazoezi katika kuibua na kuviendeleza vipaji hivyo.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa mazoezi, ndio maana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, akatangaza tarehe mosi Januari ya kila mwaka kuwa siku ya mazoezi Zanzibar.

Katika kuunga mkono vikundi hivyo vipya, Maalim Seif aliahidi kuchangia shilingi milioni mbili na laki moja kwa ajili ya vikundi saba alivyovizindua na kuvikabidhi vyeti kwa kuendelea na mazoezi.

Mapema akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk, amesema Wizara yake itakuwa mstari wa mbele kushirikiana na vikundi vya mazoezi nchini.

Uzinduzi huo ulitanguliwa na maandamano ya vikundi kadhaa vya mazoezi kutoka Kisiwani Pemba yalianzia barabara ya Baraza la Wawakilishi Pemba hadi Skuli ya Kizimbani, na baadaye kufanyika mazoeni ya viungo pamoja na mashindano ya kuvuta kamba na mbio za magunia.

0 comments:

 
Top