Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba yapo mapungufu mengi katika Sekta ya Elimu yanayoendelea kuleta changamoto kwa Walimu na wanafunzi katika skuli mbali mbali hapa nchini ambayo ufumbuzi wake ni mashirikiano kati ya Serikali, Jamii yenyewe na washirika wa maendeleo.
Alisema juhudi za pamoja zinahitajika katika kupambana na mapungufu hayo ili kwenda sambamba na Karne hii ya 21 inayohitaji maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kupata mahitaji katika kuendeleza harakati za kila siku za jamii.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi Vikalio 25 kwa wanafunzi wa Skuli ya Fujoni iliyopo Wilaya ya Kaskazini” B” akitoa ahadi pia ya kukamilisha idadi ya mahitaji kamili ya vikalio 60 kwa skuli hiyo katika kipindi kifupi kijacho.
Alisema hakuna changine chochote kwa sasa katika dunia hii kutokana na mabadiliko ya mfumo wa Sayansi na Teknolojia isipokuwa Elimu ambayo ndio ufunguo wa kila kitu.
“ Hakuna choichote katika Dunia hiio zaidi ya elimu ambayo ndio ufunguo wa kila kitu “. Alisisitiza Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.
Balozi Seif aliwaasa wanafunzi wa skuli hiyo pamoja na nyengine hapa Nchini watengeneze maisha yao ya baadaye kwa kujituma zaidi katika kutafuta elimu bora inayokwenda sambamba na ulimwengu wao wa sayansi na teknolojia.
Alisema mfumo uliopo sasa unawalazimisha wanafunzi kusoma kwa ziada wakielewa kwamba wao ndio warithi wa kuliongoza Taifa hili katika Nyanja na nyadhifa mbali mbali zilizopo kwenye tekta za umma na hata zile binafsi ambazo zinahudumia jamii.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Fujoni pamoja na walimu wa Skuli hiyo kwa kazi kubwa wanazoendelea kuzitekeleza za kuleta maendeleo ya skuli.
Alifahamisha kwamba wanafunzi wa darasa la kumi na tatu na kumi na Nne wa Skuli hiyo wanaoendelea na masomo yao katika skuli hiyo ni sehemu ya mafanikio ya juhudi za Kamati ya Skuli pamoja na walimu hao.
Mapema Afisa Tawala wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Juma Abdulla Hamad alisema Wilaya hiyo inaendelea kupata faraja kubwa kutokana na juhudi ya ziada inayochukuliwa na Mbunge wa Jimbo la Kitope katika kusaidia sekta mbali mbali za jamii hasa ile ya elimu na huduma za maji safi na salama.
Nd. Juma alisema juhudi hizo muhimu zimekuwa zikiwaondoshea changamoto wananchi na wanafunzi sio wa Jimbo la Kitope pekee bali hata wale wa Vijiji vya jirani na waliomo ndani ya Wilaya hiyo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Fujoni pamoja na walimu na Wanafunzi wa skuli hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bwana Abdullah Ali Juma amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kitope kwa mchango wake mkubwa alioutoa wa kusaidia mdeski kwa skuli hiyo.
Bwana Abdulla alisema katika kuunga mkono jitihada za Mbunge huyo alimuahidi kwamba vikalio hivyo vitatumiwa katika utaratibu utakaoviwezesha kudumu kwa kipindi kirefu zaidi.
Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi tayari ameshakabidhi vikalio kwa Skuli za Upenja na Kiwengwa akitekeleza ahadi aliyoitoa kwa Viongozi na walimu wa skuli hizo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment