Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif li Iddi amewanasihi akina mama Nchini kwamba mwaka huu ni wa kupata kile wanachokihitaji kwa karne nyingi zilizopita katika kuongeza kasi ya ushiriki wao kwenye uchaguzi Mkuu ujao unaojenga mazingira yao katika mamlaka ya maamuzi ya Taifa hili.

Alisema wakipoteza fursa hii mwaka huu inaweza kuwachukuwa miaka mingi ijayo kupatikana kwake kwa vile wasiopenda maendeleo ya Wanawake bado wapo ndani ya Taifa hili.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akilifungua Kongamano la Mwanamke na Uongozi katika Katiba inayopendekezwa lililoandaliwa na Taasisi ya Mwanaharakati Siti Binti Saad lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Grand Palace Kinu cha Taa Malindi Mjini Zanzibar.

Alisema mara nyingi wanaume kwa kupendelea kuendeleza mfumo dume wako mstawi wa mbele kupinga wanawake kupata haki zao kama inavyoshuhudiwa hivi sasa hapa nchini katika kipindi hichi cha mpito kuelekea kwenye kura ya maoni.

Balozi Seif lifahamisha kwamba ipomiofano inayoonyesha wazi kwamba wana harakati na wanamageuzi katika maeneo mbali mbali Duniani imewachukuwa takriban miaka zaidi ya 100 ya kupata haki wanawake katika kupiga kura kama wanaume.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa Utafiti katika fani ya Uongozi inaonyesha kwamba taasisi zenye Uongozi ulio sawa kijinsia hufanya vyema ikilinganishwa na zile zinazoendeshwa na kutawaliwa na mfumo dume.

Alisema Taifa ya Tanzania imeliona tatizo hili na tayari imejaribu kulitafutia ufumbuzi kwa kupendekeza Katiba Mpya inayotoa nafasi kwa akina mama kushiriki sawia na wanaume katika vyombo vya maamuzi kama Bunge.

“ Bila shaka tyunaamini Bunge la Hamsini kwa Hamsini litakuwa na ufanisi zaidi kuliko bunge la sasa hivi. Hali kama hiyo tunaamini itakuwepo pia kwenye vyombo vyengine vya kupitisha maamuzi kama Baraza la Mawaziri na Kadhalika “. Alifafanua Balozi Seif.

Alisema kitwakimu idadi ya Wanawake hapa Nchini bado ni kubwa kwa asilimia 51% ikilinganishwa na wanaume. Hivyo uwezekano wa kupita kirahisi Katiba iliyopendekezwa ni kiubwa zaidi iwapo akina mama hao watajitokeza kwa wingi kuipigia kura ya ndio.

Balozi Seif alisisitiza kwamba Katiba iliyopendekezwa endapo itafanikiwa kupita itasaidia kufungua milango mingi ya fursa za Uongozi kwa akina mama walio wengi hapa Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wanawake Nchini kujipanga vizuri katika kushika nafasi mbali mbali za uongozi wa Taifa hili lakini cha msingi kwao hilo litafanikiwa endapo wataamua kujitokeza kuomba nafasio hizo.

Alisema kama ilivyokuwa muhimu kujitokeza kwao kuomba kuchaguliwa lakini muhimu pia kuchagua wagombea wanaowapenda ambao watajikita zaidi katika kukubali kuwatumikia.

“ Mkikosea mwaka huu kumchagua kiongozi asiyefaa, ina maana kwamba mtakuwa mmekosea kwa kipindi cha miaka mitano ijayo “. Alitahadharisha Balozi Seif.

Balozi Seif aliitanabahisha jamii kwamba kuibeza Katiba iliyopendekezwa ni sawa na kubeza juhudi za wanawake walizochukuwa miaka mingi iliyopita katika kudai haki zao na hatimae kufanikiwa kuziingiza katika sheria mama ya nchi ambayo ni Katiba iliyopendekezwa.

Aliwashauri akina mama kuwapuuza akina Baba hao hata kama wanatoka katika vyama wanavyovipenda au Taasisi za Kidini au zile za kiraia wanazozifuata na badala yake watumie busara alizozichukuwa Mwanaharakati Siti Binti Saad.

Alisema jibu sahihi la kebehi na jeuriza zinazoendelea kutolewa na baadhi ya akiba Baba ni kwa akina mama hao kutumia busara kwa kuipigia kura ya ndio Katiba inayopendekezwa.

Balozi Seif alieleza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 57 ya Katiba inayopendekezwa zipo haki kadhaa za wanawake zitakazosaidia kuondoa baadhi ya mfumo dume iliokuwa ukiwakandamiza kwa miaka kadhaa iliyopita.

Alizitaja baadhi ya haki hizo kwa mujibu wa ibara hiyo y 57 kuwa ni pamoja na kuheshimiwa, kuthaminiwa na kutambuliwa utu wa mwanamke, kulindwa dhidi ya ubaguzi, udhalilishwaji, dhulma, unyanyasaji, ukatili wa kijinsia na mila potovu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad kwa juhudi zake ilizochukuwa katika kuandaa kongamano hilo la Mwanamke na Uongozi katika Katiba inayopendekezwa.

Balozi Seif alisema si rahisi kwa Taasisi change kama hiyo kufanya mambo makubwa kama hayo lakini imeonyesha pamoja na uchanga huo imeweza kufanya masuala mazito ya kupigiwa mfano.

Mapema Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanaharakati Siti Binti Saada Bibi Nasra Moh’d Hilal aliwatanabahisha akina mama wenzake kwamba huu ni wakati mzuri kwao kuitumia nafasi iliyokuwemo ndani ya Katiba iliyopendekezwa katika kujiimarisha kiuongozi.

Bibi Nasra alisema njia pekee katika kuhakikisha wana wake hao wanaitumia fursa hiyo ni kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kupiga kura ya maoni sambamba na ushiriki wa uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top