Na: Khamis Haji (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania wana mchango mkubwa katika kuisaidia Zanzibar kubaki katika hali ya amani na utulivu na kuwawezesha wananchi kujiletea maendeleo.
Maalim Seif amesema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Jaap Frederiks huko ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.
Maalim Seif amesema licha ya kuimarika kwa hali ya amani na mshikamano, tokea kuanzishwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, bado vinajitokeza viashiria vinavyoweza kuteteresha hali hiyo, iwapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa, hasa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesema miongoni mwa masikitiko makubwa ya wananchi wengi hasa vijana ni kunyimwa haki zao, ikiwemo vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, huku baadhi ya watu ambao hawana sifa wakipatiwa vitambulisho hivyo.
Amesema kitendo cha baadhi ya watu kunyimwa haki ya kupata vitambulisho kinaashiria ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na kinaweza kusababisha hali ya utulivu kutetereka.
Maalim Seif amesema Mabalozi wanayo nafasi ya kuzungumza na viongozi Serikalini pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, ili kasoro zinazojitokeza ziweze kupatia ufumbuzi na hatimae wananchi wote waweze kupata haki zao bila ya kubaguliwa.
Naye Balozi Frederiks amemueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa, Jumuiya ya Kimataifa inaiheshimu sana Zanzibar kutokana na uwezo mkubwa iliouonesha kuleta amani na utulivu kupitia maridhiano ya kisiasa yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Amesema kwa miaka mingi na zaidi inapofika wakati wa uchaguzi Zanzibar ilikuwa ikikumbwa na vurugu, hali ambayo haikufurahiwa na Jumuiya ya Kimataifa, na kwamba kurejea tena kwa hali hiyo itakuwa ni kosa kubwa na hali hiyo haipaswi kuachiwa.
Amesema kutokana na hali hiyo wataendelea kusaidia juhudi za kuhakikisha hali iliyopo ya amani, utulivu na mashikamano inadumu kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar bila ya kujali tafauti zao.
Balozi huyo amesema Zanzibar hivi sasa imekuwa kimbilio la watalii kutoka mataifa mbali mbali, baada ya watalii hao kuridhishwa na hali ya amani na utulivu iliyopo, ikilinganishwa na nchi nyingi Barani Afrika ambazo zimekumbwa na migogoro na mapigano.
Amesema uamuzi wa watalii kuja Zanzibar ni baada ya kushawishika na hali ya amani na utulivu iliyopo, na ameonya iwapo hali hiyo itatetereka kwa sababu zozote zile ikiwemo uchaguzi, watalii hao wanaweza kuondoka Zanzibar na kusababisha athari kubwa za kiuchumi na kimaendeleo.
0 comments:
Post a Comment