Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba Kiongozi ye yote atakayemzuia Mwananchi kupiga kura iwe ya Maoni na hata ile ya Uchaguzi Mkuu aelewe kwamba anamnyima fursa ya Kidemokrasia Mwananchi huyo.
Alisema Wananchi wakati wote wanahitaji kupata mabadiliko ya maendeleo yatakayompua muelekeo mzuri wa kuendelea kuimarisha na kustawisha ustawi wa maisha yake ya kila siku.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati akizungumza na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi pamoja na wananchi wa Jimbo la Nungwi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Tawi la CCM la Kijiji hicho baada ya kuweka jiwe la Msingi la DR. Omar Ali Juma Maskani.
Shughuli hiyo ilikwenda sambamba na Balozi Seif kukabidhi Seti za TV, Dvd na CD kwa Maskani kumi na Moja za Jimbo la Nungwi pamoja na Seti za Jezi na Mipira kwa Timu 9 za Jimbo hilo akiahidi pia kuzipatia Ving’amuzi Maskani zote zilizopata msaada huo.
Balozi Seif aliwakumbusha wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Nungwi kutofanya makosa kama waliyoyafanya mwaka 2010 na badala yake waongeze nguvu katika kuhakikisha CCM inarejea kuliongoza Jimbo hilo lililoazimwa kwa upinzani.
Alisema hakuna mbadala katika ushindi wa Chama cha Mapinduzi kwa mwaka huu wa uchaguzi ambao chama hichokimelenga kuuzika kabisa upinzani uliopo hapa nchini na kubakia kuwa Historia ya Kisiasa Nchini Tanzania.
Akizungumzia huduma muhimu zinazopaswa kupatiwa Wananchi Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaambia Wananchi hao wa Nungwi na Zanzibar kwa ujumla kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaiagiza Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } kuziondoa Mita zote za Tukuza zilizofungwa katika Visima vya Maji.
Alisema hatua hiyo ya Serikali iliyojadiliwa na kuamuliwa na Baraza la Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Dr. Ali Moh’d Shein imelenga kuwaondoshea usumbufu wa kupata huduma za maji safi na salama wananchi wote wa Visiwa vya Unguja na Pemba.
Naye Mke wa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Mama Asha Suleiman Iddi aliwatahadharisha Wananchi kujiepusha na mbinu na ujanja wa wanasiasa matepeli wanaopita Mitaani kuwadanganya siku hadi siku.
Mama Asha alisema Viongozi wengi wa Kisiasa wenye tabia hiyo ya kutapeli wananchi na hasa wanachama wao huzingatia kujinufaisha wao binafsi bila ya kufikiria kero na changamoto zinazowakabili wananchi wanaowadanganya na hatma yake ni kuwaongezea umaskini.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM { UVCCM } Zanzibar Shaka Hamdu Shaka akiwakumbusha Vijana wa Nungwi wajibu wao wa kulinda maslahi ya wananchi wa Taifa hili aliwahimiza kujiandaa na harakati za ushindi wa CCM inayotarajiwa kuendelea kuongoza Dola ya Tanzania baada ya uchaguzi wa Mwezi wa Oktoba mwaka huu.
Shaka alisema Vijana kama nguzo ya Chama cha Mapinduzi kupitia Jumuiya yao ya Vijana ndio wenye kujumu na wajibu wa kuhakikisha ushindi wa Chama hicho kwenye uchaguzi Mkuu ujao unakuwa wa kishindo na kushuhudiwa na jumuiya za Kimataifa.
Vifaa vyote vilivyotolewa na Kukabidhiwa kwa Maskani 11 na Timu 9 za Jimbo la Nungwi ikiwemo Seti za TV, dvd’s, C.D, Seti za Jezi na Mipira zimegharimu jumla ya shilingi Milioni kumi na Mbili { 12,000,000/- }.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment