Na: Hassan Hamad, Doha.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ameishauri serikali ya Qatar kuangalia uwezekano wa kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza sekta ya nishati nchini.

Amesema Zanzibar ikiwa miongoni mwa nchi zinazoendelea, bado inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya upatikanaji wa umeme wa uhakika ambapo kwa sasa inategemea nishati hiyo kutoka Tanzania Bara.

Maalim Seif ametoa ushauri huo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nishati na Viwanda wa Qatar Dr. Mohammed Saleh Al-Sada, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake nchini humo.

Amesema wakati umefika kwa Zanzibar kuwa na vyanzo vyake vya umeme, na kwamba serikali imo katika mkakati wa upatikanaji wa vyanzo mbadala vya umeme, ili kuhakikisha kuwa huduma hiyo inakuwa ya uhakika.

Amemueleza Wariri huyo na ujumbe wake kuwa licha ya Zanzibar kutokuwa na mito ya kuzalisha nishati hiyo, lakini inaweza kupatikana kupitia nguvu za jua na upepo ambapo baadhi ya tafiti zimeshabaini uwezekano wa upatikanaji wake.

Hivyo amesema Qatar ikiwa nchi yenye uzoefu mkubwa katika sekta ya nishati, inayo fursa ya kushirikiana na Zanzibar ili kuhakikisha kuwa visiwa vya Unguja na Pemba vinakuwa na vyanzo vyake vya umeme na kuifanya huduma hiyo kuwa ya uhakika.

Maalim Seif ametaja changamoto nyengine inayoikabili Zanzibar kuwa ni ukosefu wa ajira kwa vijana, hali inayotishia mustakbali wa maendeleo ya vijana hao ambao wengi wao tayari wamepata elimu ya sekondari hadi kufikia vyuo vikuu.

Katika mazungumzo hayo Waziri wa Nishati na Viwanda wa Qatar Dr. Mohammed Saleh Al-Sada, ameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka utaratibu mzuri kwa wawekezaji wa sekta mbali mbali, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu yake.

Uchumi wa Qatar unategemea zaidi sekta ya mafuta na gesi asilia ambayo huchangia zaidi ya asilimia 70 ya pato la taifa hilo linalokua kwa kasi kiuchumi.


Kabla ya kukua kwa sekta ya mafuta na gesi asilia takriban miaka 40 iliyopita, Qatar ilitegemea sekta ya uvuvi na ilikuwa miongoni mwa nchi maskini, lakini katika kipindi cha hivi karibuni imeibuka kuwa nchi tajiri kabisa duniani kwa kipato cha wananchi (per capita), na pia yenye maendeleo makubwa zaidi ya wanachi katika ulimwengu wa nchi za kiarabu.

0 comments:

 
Top