Na: Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameshauri sheria ya kuwaenzi waasisi wa Taifa ifanyiwe marekebisho, ili kuiwezesha bodi ya udhamini wa mfuko wa kuwaenzi waasisi hao kufanya kazi zao kwa uhakika.

Amesema sheria hiyo namba 18 ya mwaka 2004, bado haijabainisha vyanzo vya mapato ya kuendesha bodi hiyo, na kutanabahisha kuwa bila ya kufanya hivyo, bodi inaweza kukabiliwa na wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yake.

Maalim Seif ametoa ushauri huo wakati akizungumza na bodi hiyo iliyofika nyumbani kwake Mbweni kwa ajili ya kujitambulisha.

Amefahamisha kuwa sheria hiyo ingepaswa kubainisha vyanzo vyake vya mapato zikiwemo Serikali ambazo zinatakiwa kutoa msukumo katika kufanikisha ustawi wa bodi hiyo.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake itatoa kila aina ya ushirikiano na msaada unaohitajika ili kuhakikisha kuwa bodi hiyo inatekelza majukumu yake kwa ufanisi.
Akizungumzia juu ya dhana ya kuwaenzi waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, amesema ni muhimu kwani viongozi hao walifanya kazi kubwa ya kuongoza mapambano dhidi ya watawala.

Amesema viongozi waasisi ni kielelezo cha Taifa, hivyo kuna kila sababu ya kuwaenzi, na kuhakikisha kuwa historia zao zinatunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo na historia ya nchi kwa ujumla.

Hata hivyo amesema jitihada zaidi zinahitajika katika kuendeleza historia ya waasisi hao na taifa kwa ujumla, sambamba na kuwafundisha vijana ili waweze kufahamu historia ya nchi yao.

Mapema akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa bodi hiyo ya udhamini wa mfuko wa kuwaenzi waasisi wa Taifa, Kanali mstaafu Kabenga Nsa Kaisi, amekiri kuwa Mfuko huo wenye lengo la kuwakumbuka na kuwaenzi waasisi wa Taifa la Tanganyika na Zanzibar, unakabiliwa na ukosefu wa vyanzo vya mapato.

Aidha ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia mafunzo wajumbe wa bodi hiyo katika nchi zenye uzoefu wa kutunza historia, ili kuongeza uelewa wa namna ya kuendeleza historia ya Tanzania na waasisi wake.

Nae mjumbe wa bodi hiyo Mama Fatma Karume, amesema serikali ina nafasi kubwa ya kuijengea uwezo bodi hiyo, katika kuhakikisha kuwa histori za waasisi wa Taifa zinaendelezwa.

“Tusisahau historia yetu, ni msingi wetu”, alisisitiza mjumbe mwengine wa bodi hiyo Dkt. John Magoti, wakati akitoa neon la shukrani.

0 comments:

 
Top