Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba msimamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Baraza lake la Mapinduzi wa kulitumia shamba lake la Kilimo liliopo Makurunge Bagamoyo Mkoa wa Pwani ni ule ule wa kuendeleza Mifugo na Kilimo.
Alisema uamuzi huo umezingatiwa kwa makusudi kuheshimu wazo la pamoja lililoibuliwa kati ya Rais wa Kwanza wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere na Rais wa Awamu ya Pili ya Zanzibar Mh. Aboud Jumbe Mwinyi la kuipatiwa Zanzibar eneo la Mifugo na Kilimo Tanzania Bara ili kuimarisha Sekta hizo.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati alipofanya ziara maalum ya kulikagua shamba la Mkurunge akiambatana na Waziri wa Kilimo, Ushirika na Chula wa Bara Mh. Steven Wasira, Naibu Waziri wa Ardhi Bara Mh. Angeja Kairuki, Waziri wa Ardhi Zanzibar Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban, Waziri wa Kilimo Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya, Makatibu Wakuu wa Wizara hizo pamoja na watendaji waandamizi wa Serikali zote mbili.
Alisema Shamba la Makurunge Bagamoyo lina Historia ndefu iliyoasisiwa na Marais waliopita ikilenga kuimarisha Muungano uliopo kati ya Tanganyika na Zanzibar sambamba na kuipa nguvu Zanzibar kwa shughuli zake za kuongeza uzalishaji katika Sekta ya Mifugo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Zanzibar imekuwa na eneo dogo la ardhi kwa kuendeleza sekta ya Kilimo na Mifugo huku idadi ya wakaazi wake ikiendelea kuongezeka kiwango ambacho kinastahiki kujengewa mindo mbinu ya maisha katika uzalishaji Kiuchumi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar Chini ya Chuo cha Kilimo Kizimbani kilichokabidhiwa shamba hilo.
Alisema ushirikiano huo muhimu kwa kiasi kikubwa ndio utakaowezesha kusadia sana hatma ya shamba hilo ambalo limekuwa na changamoto ya kuvamiwa na baadhi ya Watu kwa shughuli za Kilimo pamoja na ujenzi wa Makazi.
Alisema lile lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuomba kupatiwa shamba hilo kutoka Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni vyema ukazingatiwa na kuheshimiwa na watu wanaolizunguuka eneo hilo.
Akitoa Taarifa ya Historia ya Shamba la Makurugne hapo Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mkuu wa Wilaya ya Magamoyo Nd.Majid Hemed Mwanga alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliomba eneo la ufugaji wanyama kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mapema mwaka 1977.
Nd. Mwanga alisema Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mali Asili ilitoa Barua rasmi Mwezi Febuari mwaka huo huo wa 1977 wa kuipatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar eneo la Shamba hapo Makurunge Bagamoyo lenye ukubwa wa Hekta 28,099.
Alisema kazi hiyo ilikwenda sambamba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwalipa fidia wananchi 64 waliokuwa na mali na vipando vyao kwenye eneo hilo ambapo watu 16 waliohusika na zoezi hilo walikataa kulipwa fidia hizo.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Bagamoyo alieleza kwamba kufifia kwa shughuli za uzalishaji wa Mifugo katika shamba hilo zilizokuwa zikifanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kulitoa fursa kwa wawekezaji kujitokeza kuomba eneo hilo kwa shughuli za uwekezaji.
Alifafanua kwamba mazungumzo ya pamoja kati ya Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yalifanyika na ukapatikana uamuzi wa kuipatia Kampuni ya Miwa ya Bagamoyo Eco Energ eneo la Hekta 22,000 kulima miwa kwa ajili ya uzalishaji wa Sukari.
Hata hivyo Nd. Mwanga alieleza kwamba zipo changamoto kadhaa zilizojitokeza kwenye shamba hilo ukiwemo uvamizi wa ujenzi na kilimo uliofanywa na watu wapatao 400 ndani ya shamba hilo.
Akizungumza katika kikao cha kutathmini ziara hiyo kwenye Hoteli ya Bagamoyo Oceanic Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kwamba Wilaya ya Bagamoyo imo ndani ya mpango wa Serikali wa kulifanya eneo hilo kuwa ukanda wa Uwekezaji Kiuchumi { EPZ }.
Mhandisi Ndikilo alisema ipo haja ya makusudi ya kuwepo kwa vikao vya mara kwa mara vya pamoja kati ya Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Uwekezaji vitega uchumi { ZIPA } na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ili kuwa na mtazamo wa pamoja utakaokwenda sambamba na mpango huo.
Alisema mtazamo huo utajenga hatma njema ya matumizi sahihi ya Ukanda huo wa Bagamoyo likiwemo eneo la shamba hilo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar liliopo Makurunge.
Mapema asubuhi katika Kikao cha Maandalizi ya ziara hiyo kiliochofanyika katika Makazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar yaliyopo Bara bara ya Haile Sellassie Jijini Dar es salaam Kamishna wa Ardhi wa Tanzania Bara Nd. Moses Msilika alisema kwamba mabadiliko ya kiuchumi katika mipango miji ya Serikali yameifanya Wilaya ya Bagamoyo kuingia katika ramani ya uwekezaji.
Nd. Moses alisema shamba la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar liliopo Makurunge limeshapimwa rasmi na kueleweka vyema mipaka yake na limeshindwa kutumiwa kwa mujibu wa mipango miji kutokana na kuwa liko chini ya mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment