Na: Khamis Haji (OMKR).

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Fionnuala Gilsenan amevihimiza vyama vikuu vya siasa Zanzibar kuendeleza utamaduni wa kuzungumza na kuzipatia ufumbuzi kasoro zinazojitokeza ili Zanzibar iendelee kubaki katika hali ya amani, umoja na mshikamano.

Ametoa ushauri huo alipofanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza was Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad yaliyofanyika nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Balozi Gilsenan amesema Zanzibar imejipatia sifa kubwa kutokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa na vyama viwili hivyo vya CCM na CUF na baadaye kuweza kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeipatia sifa kubwa Zanzibar kutokana na mafanikio makubwa yaliyojitokeza ikiwemo hali ya utulivu na kusababisha wananchi wa Zanzibar kuwa wamoja na kuelekeza nguvu zao katika kujiletea maendeleo.

Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesifu mahusiano mema yaliyopo baina ya Zanzibar na Ireland ambayo yamewawezesha wananchi kunufaika na miradi mbali mbali ya maendeleo, kiuchumi na kijamii, ikiwemo ufugaji wa ng’ombe wa kisasa kisiwani Pemba.

Maalim Seif amesema ipo haja mahusiano hayo yaendelezwe katika nyanja nyengine, ikiwemo sekta za biashara, kilimo, utalii na viwanda vidogo vidogo, maeneo ambayo amesema yana mchango mkubwa katika kuinua uchunmi wa Serikali na wananchi mmoja mmoja.

Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Maalim Seif amesema utaratibu huo ni mzuri na umeonesha mafanikio makubwa Zanzibar na hauna budi kuendelezwa katika ngazi zote.

Maalim Seif amesema kinachohitajika hivi sasa ni elimu zaidi kwa viongozi hasa wa ngazi za chini, kuanzia mikoa, Wilaya na Shehia ili waelewe umuhimu wa Serikali ya Umoaj wa Kitaifa na waweze kutekeleza majukumu yao bila ya upendeleo miongoni mwa wananchi wote.

Maalim Seif amesema miongoni mwa kasoro zinazolalamikiwa sana ni baadhi ya wananchi wa Zanzibar wenye sifa kunyimwa haki yao ya kupata vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, licha ya juhudi kubwa wanazozichukua kuviomba katika mamlaka husika.

Amesema kasoro kama hizo hazina budi kushughulikiwa kwa haraka kuepusha dhana kuwa baadhi ya watu wanabaguliwa kwa misingi ya itikadi za kisiasa.

Kuhusu hali ya uchumi Maalim Seif amesema Zanzibar inapiga hatua licha ya kuwa sekta zake za kiuchumi zikiwemo Utalii na zao la karafuu zimekuwa zikipata mabadiliko kulingana na mabadiliko ya misimu.

“Unajua uchumi wetu unategemea zaidi sekta za utalii na zao la karafuu, lakini sekta hizi hutegemea misimu. Kwa mfano msimu huu wa karafuu tunaweza kupata mavuno mazuri lakini misimu miwili inayofuata mavuno hupungua, na hivyo hivyo kwenye sekta ya utalii”, Maalim Seif alimueleza balozi huyo.

Hata hivyo amesema wananchi wamehamasika katika sekta hizo hasa zao la karafuu, baada ya kuona kuwa zinawaletea tija, na kwamba jumla ya miche milioni moja ya mikarafuu hutolewa kwa wakulima kila mwaka ili kuliendeleza zao hilo.

0 comments:

 
Top