Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wote inazingatia kuunga mkono nguvu za Vijana waliojikubalisha kukusanyika pamoja katika kutafuta maarifa ya kuendesha miradi yao ya kiuchumi kwa njia ya vikundi tofauti ili waendeshe maisha yao vizuri.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akilifunguwa Darasa la wajasiri amali wa fani mbali mbali kutoka majimbo Matatu ya Wilaya ya Kaskazini “B” hapo katika banda la uuzaji wa Karafuu Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif aliwaeleza Vijana hao wapatao Mia 770 wa Majimbo ya Mahonda, Bumbwini na Kitope kwamba hakuna fani hata mmoja isiyohimili ajira, lakini cha kuzingatia zaidi ni kujizatiti katika kukabiliana na changamoto zilizopo.
Alisema walioamua kujikusanya pamoja katika kuchangamkia maisha ndio wanaostahiki kuwezeshwa kwa kupatiwa vitendea kazi na misaada kutoka Serikalini pamoja na washirika wa maendeleo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema juhudi za makusudi atalazimika kuzifanya kwa kuzungumza na Waziri anayesimamia masuala ya uwezeshaji kiuchumi ili itafutwe njia itakayoweza kuwasaidia Vijana hao ambao tayari wameshaamua kujitegemea kiuchumi.
“ Mmenipa moyo kwa kitendo chenu cha kujikusanya pamoja katika kuhangaikia maisha mkielewa wazi kwamba fursa za ajira Serikalini hivi sasa ni mtihani. Hatua hii imenishawishi niongee na Waziri wa Uwezeshaji ili ipatikane njia ya kukusaidieni “. Alieleza Balozi Seif.
Aliwatahadharisha na kuwaonya vijana hao kuzingatia mambo yenye faida kwao badala ya kufuata wimbi la kupotoshwa na wanasiasa wenye nia ya kuwatumia vijana hao katika kukamilisha malengo yao.
Katika kuunga mkono juhudi za Vijana hao Balozi Seif alihamasika kuchangia vyarahani sita, vitambaa Majora Sita, nyuzi na Mikasi kwa wale Vijana wa fani ya darasa la ushoni vifaa ambavyo vitawasaidia katika kufanya mazoezi kwa vitendo kwenye masomo yao.
Hata hivyo Balozi Seif aliwaomba wale Vijana wa fani nyengine kwenye darasa hilo la wajasiri amali mbali mbali kuorodhesha mahitaji yao muhimu muda huu mfupi katika masomo yao ili apate wasaa wa kuyafanyia kazi maombi yao.
Alisema kinachohitajika kwa sasa ili kuona darasa hilo linaendelea kufanikiwa vyema ni upatikanaji wa vifaa vitakavyokuwa mkombozi katika masomo yao ya vitendo.
Mapema Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi aliwashauri vijana hao hasa wale wasichana wanapomaliza masomo yao kujikusanya pamoja katika vikundi vya ushirika ili waanze vyema katika maisha yao ya baadaye.
Mama Asha alisema wanawake ndio watu wa mwanzo wanaopambana na matatizo katika harakati zao za kimaisha baada ya mzigo mkubwa kuachiwa na waume zao.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alilitembelea na kujikagua jengo la Madrasat Al – Mujitahidin liliopo katika Kijiji cha Makoba liliomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.
Akikabidhi vifaa kama saruji, Mafeni pamoja na fedha taslimu shilingi Laki 400,000/- za kukamilishia huduma za upatikanaji wa Umeme vilivyoahidiwa kutolewa na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Balozi Seif alisema kazi iliyofanywa na wananchi wa Makoba ya kujenga Madrasa kwa ajili ya kizazi chao inafaa kuungwa mkono na Jamii.
Balozi Seif alisema nyumba za Ibada kama msikiti na madrasa zinazofundisha Mila, silka,Utamaduni pamoja na mafunzo ya dini lazima ziheshimike kwa kupewa hadhi inayolingana na dini yenyewe.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahimiza waumini hao wa dini ya Kiislamu wa Makoba kuwa makini katika kujifunza elimu ya Dini wakilenga zaidi kuwapatia taaluma hiyo watoto wao.
Akisoma risala ya wananchi na waumini hao wa dini ya Kiislamu wa Wadi ya Makoba Diwani wa Wadi hiyo Ndugu Juma Zahor Juma alisema ujenzi wa Madrasa hiyo ulioanzishwa kwa michango ya waumini na wananchi wenyewe ulianza mwaka 2003.
Nd. Juma alisema hatua hiyo imekuja kutokana na ufinyu wa mahali pa kuwahifadhi wanafunzi wa Madrasa hiyo wakati wa kupatiwa taaluma ya elimu na mafunzo ya Dini.
Aliwapongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi kwa moyo waliouonyesha wa kusaidia nguvu katika harakati za ujenzi wa jengo hilo la kudumu la Madrasat Al – Mujitahidin.
Hata hivyo Diwani huyo wa Wadi ya Mkoba alifafanua kwamba bado ipo changamoto inayoikabili Madrasa hiyo akitaja kuwa ni ujenzi wa vyoo ili kuhifadhi mazingira.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment