Karibu nusu ya wananchi (46%) wameripoti kuwahi kushuhudia ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu katika ajira. Wakati huo huo, ni wananchi wawili tu kati ya kumi (17%) waliokiri kufahamu asasi/mashirika yanayotoa upendeleo kwenye suala la kuwaajiri watu wenye ulemavu. Wananchi waliripoti kuwa miongoni mwa mashirika haya asilimia 38 ni taasisi za kiserikali. 

Vile vile wananchi waliripoti kuwafahamu watoto wenye umri wa kwenda shule ambao ni walemavu ila hawakuwa shuleni. Mwananchi mmoja kati ya watatu alisema anamfahamu mtoto mwenye umri wa kusoma shule ya msingi, na wawili kati ya kumi waliwajua watoto wenye umri wa kusoma shule ya sekondari lakini hawakuwa shule.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Kulinda haki za kila mtu: Maoni ya wananchi juu ya ulemavu. Muhtasari huu umetokana na Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kupitia simu ya mkononi. Utafiti huu hukusanya taarifa kwenye kaya zote Tanzania Bara. Takwimu zilikusanywa mwezi Julai 2014.

Matokeo haya yameyotokana na mitazamo ya wananchi yanayoibua kwa undani ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu ama moja kwa moja au kwa kupitia kukosekana kwa huduma na ajira.

Wananchi walikuwa na mtazamo ulioonesha kuwa wanawajali watu wenye ulemavu. Idadi kubwa ya wananchi (91%) waliripoti kuwa wanawaona watu wenye ulemavu kama watu wanaohitaji kutunzwa. Vile vile mwananchi mmoja kati ya watatu aliripoti kuwaona watu wenye ulemavu kama siyo watu kamili (33%) au kuwa ni watu ambao ni kikwazo kwao (32%). Karibu nusu ya wahojiwa (46%) wanawaona watu wenye ulemavu kama mzigo kiuchumi kwa familia zao na ni wananchi wanne kati ya kumi (39%) wanaowaona kama watu wenye uzalishaji mdogo kuliko watu wasio na ulemavu.

Licha ya maoni haya mkanganyiko, kuna idadi kubwa ya wananchi ambao wanawaona watu wenye ulemavu kama watu sawa na wengine (62%). Wananchi wameripoti kuwa watu wenye ulemavu wanaweza kushika nafasi za uongozi kwenye taasisi za dini (88%), biashara (87%) na jamii (85%). Aidha, wananchi sita kati ya kumi (58%) wanaamini kuwa watu wenye ulemavu wana fursa sawa na wengine.

Wananchi pia wanaunga mkono hatua zinazochukuliwa kuhakikisha fursa zinapatikana kwa watu wenye ulemavu. Walipoulizwa kuhusu viti vilivyotengwa Bungeni kwa ajili ya watu wenye ulemavu, karibu wananchi wote (97%) wanafikiri idadi iongezwe, wanaotaka viongezwe kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu ya pili ya Katiba (29%), na wananchi (68%) wangependa viongezwe zaidi ya hapo.

Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alibainisha: "Wananchi wengi wanawaona watu wenye ulemavu kama binadamu wasiokamilika wanaohitaji msaada. Hii haisaidii. Tunahitaji kuondokana na mtazamo huu wa kuwaona watu wenye ulemavu kama waathirika au mizigo na badala yake tuwaone kama watu wenye uwezo tofauti, wanaostahili heshima na haki ya kupata fursa sawa kama raia wengine. 

Hilo linahitaji hatua angalau kwenye mambo mawili: Moja, kuweka mfumo madhubuti wa kisheria ambao utaweka fursa sawa kwenye huduma zote za Serikali na biashara. Pili, kwa mashirika yanayotetea haki za watu wenye ulemavu, vyombo vya habari na wadau wengine kuwa wasisitize uwezo wa watu wenye ulemavu, na kuwapa nafasi ya kuonesha ni nini wanaweza kufanya na ni fursa zipi wanazostahili kupata ili waweze kufanya. Hii itasaidia sana, badala ya kuonesha mapungufu yao."

0 comments:

 
Top