Uongozi wa Kisiwa cha Jimbo la Hainan Nchini Jamuhuri ya Watu wa China upo tayari kutuma wataalamu na wawekezaji wake kufungua milango ya uwekezaji katika Visiwa vya Zanzibar  katika miradi ya Kilimo, Utalii na Mazao ya Baharini kwa lengo la kusaidi maendeleo ya Zanzibar.

 Gavana wa Jimbo la Hainan Bwana Jian Dingzhi alitoa kauli  hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na ujumbe wake ambao  umenza ziara rasmi ya Kiserikali ya Siku Kumi katika Jimbo  hilo hapo Hoteli ya Le Meriden Mji Mkuu wa Kisiwa hicho wa  Haikou.

 Bwana Jiang Dinmgzhi alimueleza Balozi Seif kwamba Jimbo  hilo ambalo ni Kisiwa kiliopo ncha ya Kusini mwa China  limekuwa na utajiri mkubwa wa wataalamu wa Sekta hizo ambao  unaweza kusaidia maendeleo na uchumi wa Zanzibar.

Alisema Uongozi wakeutaandaa utaratibu na mipango ya kusaidia kutoa taaluma ya kisasa kwa wavuvi na   wakulima wa Zanzibar ili wapate fursa ya kuzalisha kitaalamu  miradi yao hali itakayowaongezea kipato na kupunguza umaskini.

 Gavana Jian Dingzhi halifahamisha kwamba hatua hiyo italenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Hainan Visiwa vinavyolingana na kufanana kimazingira.

Alielezea faraja yake kuona kwamba Kizazi kipya cha jamii ya Wananchi wa Jamuhuri ya Watu wa China kimekuwa kikijifunza uhusiano wa kidugu unaoendelea kuimarika baina ya pande hizo  mbili.

 Gavana huyo wa Jimbo la Hainan aliwashauri na kuwaomba  wafanyabiashara wa Zanzibar kulitumia soko la Hainan hasa  lile la mazao ya Baharini katika kuendeleza biashara zao. Alisema Hainan imekuwa mzalishaji mkubwa wa mazao ya Baharini yanayokadiriwa kufikia Tani 50,000 ndani yha mwaka  huu wa 2014.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi alisema Sekta za Kilimo, Utalii na  Mazao ya Baharini zimekuwa zikitoa mchango kuongeza  mapato ya Taifa.  Balozi Seif alimueleza Gavana Jian Dingzhi kwamba ziara ya Ujumbe wake ndani ya Jimbo la Hainan itatoa fursa ya  kujifunza maendeleo yaliyopatikana ambayo yameliwezesha Jimbo hilo kupata ufanisi mpana.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa shirika la Ndege la Hainan kuanzisha safari za moja kwa moja  za usafiri wa anga kati ya Visiwa hivyo kwa lengo la kupanua  wigo wa biashara hasa utalii.

 Alisema uamuzi huo endapo utafikiwa unaweza kutoa nafasi kwa  wawekezaji wa Hainan kuhamasika na hatiame kuamua kuwekeza miradi yao ya kiuchumi katika Visiwa vya Zanzibar.

“ Ziara yangu hii pamoja na mambo mengine ya ushirikiano na uhusiano kati ya Zanzibar na Hainan lakini pia imelenga  kushawishi wafanyabiashara na wawekezaji wa Hainan kuwekeza  vitega uchumi vyao Zanzibar “. Alisema Balozi Seif.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake walitembelea meneo huru ya uwekezaji  pamoja na kuangalia uzalishaji katika kiwanda cha usindikaji  Samaki kwenye mji wa Kisiwa cha Haina, Haikou.

 Akizungumza na wawakilishi wa Kiwanda hicho na ule wa Maeneo  huru ya uwekezaji wakiongozwa na Meya wa Mji waChengmai Bwana Zhaomin Ji , Balozi Seif aliwapongeza Wananchi wa Hainan kwa hatua kubwa waliyofikia katika kuimarisha  maendeleo yao.

 Balozi Seif maendeleo hayo yanatoa nafasi kwa Zanzibar  kujifunza kupitia ziara za mara kwa mara za viongozi na watendaji wake.  Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha maeneo huru ya uwekezaji pamoja na mfumo wa Bandari huru ya kiuchumi ili kuimarisha maendeleo yake lakini bado miundombinu katika maeneo hayo yangali duni.

 Naye Msaidizi wa Meya wa Mji wa Chengmai ambae pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Kamati ya Chama ya Mji huo Bwana Sitao Yang alisema Hainan ni miongoni mwa Majimbo yenye rasilmali kubwa ya kiuchumi ikitanguliwa na Taiwan, alisema uchumi wa Jimbo la Hainan umekuwa na kufikia  uwekezaji wa Yuan Bilioni 20 mwaka huu kutokana na kuimarika kwa miundo mbinu yake inayotoa fursa katika uwekezaji wa sekta ya Utalii.

Bwana Sitao alimuhakikishia Balozi Seif kwamba juhudi zitaongezwa katika kuona uhusiano wa kidugu unaendelea kuimarika kati ya Zanzibar na Hainan kwa kuweka ubia katika  miradi ya kiuchumi na maendeleo.

Wakati wa Jioni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ujumbe wake walijumuika pamoja na wajumbe wa Mkutano wa Tato wa Ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye chakula cha jionikilichoandaliwa na Gavana wa Hainan Bwana Jian Dingzhi  hapo kwenye Hoteli ya Le Meriden Mjini Haoku.

 Othman Khamis Ame
 Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top