Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Serikali wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi kuziteremsha mara moja bendera zote za Jumuiya ya Muamsho na mihadhara ya Kiislamu zilizomo ndani ya Mkoa huo.
Alisema jukumu hilo litapaswa kutekelezwa kuanzia hivi sasa chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja akishirikiana na Wakuu wa Wilaya zote mbili za Kaskazini “A” na “ B”.
Balozi Seif alitoa agizo hilo katika hafla fupi ya kukabidhi vitendea kazi kwa Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa Jimbo la Mkwajuni iliyofanyika katika uwanja wa Kituo cha Ualimu Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema Bendera zinazotambuliwa kisheria ni zile za Taasisi za Umma pamoja na Vyama vya Siasa vilivyopata usajili na ridhaa kutoka kwa msajili wa vyama vya Siasa Nchini Tanzania.
Alikemea kwamba si vyema kwa baadhi ya watu, Taasisi au Jumuiya za Kijamii zikatumia usajili wanaopewa kwa kujichukulia maamuzi yaliyo nje ya taratibu za kisheria jambo ambalo huleta sintofahamu miongoni mwa jamii.
Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliupongeza Uongozi wa Jimbo la Mkwajuni kwa umahiri wake wa kusimamia sera na Ilani za Chama Tawala.
Alisema jitihada za viongozi hao zilizolenga kuimarisha utendaji wa Chama cha Mapinduzi zimelifanya Jimbo la Mkwajuni kuwa moto wa kuotea mbali kwa kuvunja nguvu za upinzani.
Alifahamisha kwamba kazi iliyopo mbele kwa viongozi na watendaji wa CCM Jimboni humo ni kutekeleza kazi zao bila ya vizingizio vya ukosefu wa vitendea kazi vikiwemo vyombo vya usafiri.
Akigusia suala la Katiba mpya Balozi Seif alisema wajibu walionao wananchi hivi sasa ni kuhakikisha kwamba wanaipiga kura ya ndio Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba.
Balozi Seif alisema Zanzibar imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na yaliyomo ndani ya Katiba iliyopendekezwa na Bunge hilo ambayo yataipa fursa zaidi kujiimarisha katika harakati zake za kiuchumi bila ya vikwazo vyovyote kutoka Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Taznania.
Alifahamisha kwamba kero nyingi zilizokuwa zikilalamikiwa na upande wa upinzani ambazo sasa wanaendeleza kampeni ya kuzipinga zimepatiwa ufumbuzi wa kina ndani ya Katiba iliyopendekezwa.
Mapema Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni Mh. Simai Jadi na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mh. Mbarouk Wadi Mussa walisema vifaa na vitendea kazi hivyo vilivyotolewa ni awamu ya kwanza.
Walisema mipango inaendelea kutekelezwa katika jitihada za Viongozi hao kuhakikisha kwamba awamu inayofuata haitachukuwa muda mrefu kutekelezwa ili iwape fursa nzuri watendaji wa Chama Jimboni humo kutekeleza vyema majukumu yao.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na Vespa kwa makatibu wa Wadi na Jimbo, Baskeli kwa makatibu wa Matawi na Jumuiya za Chama, Vipaza sauti kwa ajili ya Wadi na misikiti, bendera kwa Mabalozi pamoja na mazulia.
Vifaa hivyo vilivyotolewa na Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo hilo la Mkwajuni vina thamani ya shilingi Milioni Thalathini na Tano { 35,000,000/ }.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment