Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kukiimarisha chuo cha Taaluma za sayansi za afya Zanzibar ili Vijana wake wawe na uwezo kamili wa kutumia taaluma yao katika kutoa huduma za afya kwa wananchi kwenye vituo mbali mbali vya afya na hospitali mjini na Vijijini hapa nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd Shein alisema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye mahafali ya 21 ya chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya zilizofanyika chuoni hapo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema kinachotekelezwa hivi sasa na Serikali katika uimarishaji wa Sekta ya afya ni usimamizi wa Ilani na Sera za Chama cha Mapinduzi zikiwemo ahadi zote zilizotolewa na chama Cha Afro Shirazy Party wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 1963 kwamba kitapokamata dola suala la matibabu litakuwa bila ya malipo kwa wananchi wote.

Rais wa Zanzibar alieleza kwamba wahitimu hao 280 wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar waliomaliza mafunzo yao ni nguvu kazi mpya inayoandaliwa katika kujenga taifa lenye afya.

Alifahamisha kwamba chuo hicho hivi sasa kimekuwa na mchango mkubwa katika kuibua wataalamu wazalendo wanaochipukia kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Taifa ya kuwaandaa walimuwa wa kusimamia mafunzo hayo.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya iliamua kuendeleza Taaluma za sayansi za Afya kwa kuanzisha rasmi chuo hicho ili kikidhi mahitaji ya Taifa kwa kupata wataalamu wa kutosha.

Aliupongeza Uongozi wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } kwa kusimamia vyema agizo la serikali la kukiongezea nguvu za uwajibikaji chuo hicho.

Alifahamisha kwamba mfumo wa kukifanya chuo hicho kuwa chini ya usimamizi wa chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar utatoa fursa wanafunzi wake kupata taaluma itakayotambuliwa Kitaifa na Kimataifa.



Alielezea matumaini yake kwamba mafunzo waliyoyapata Vijana hao wa chuo cha Taaluma za sayansi za afya watayatumia vyema katika kutoa huduma nzuri kwa jamii wakizingatia misingi bora ya kazi.

Akitoa nasaha zake kwa wahitimu hao Rais wa Zanzibar aliwasihi kufuata maadili na miiko ya kazi hasa popote watakapopangiwa kama walivyoahidi na kufundishwa na wakufunzi wao.

Alisema hatua hiyo ni miongoni mwa uwajibikaji unaozingatia nidhamu ya kazi na nivyema wakajiepusha na dhama ya kutaka kufanya kazi nje ya nchi wakisahau uzalendo wao.

Kuhusu changamoto zinazokikabili chuo hicho Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi na wanafunzi wa chuo hicho kwamba Serikali itashirikiana nayo katika kutafuta mbinu za kutatua kero hizo kwa mujibu wa uwezo uliopo.

Alisema kero kama vile mabadiliko ya mishahara liko katika hatua nzuri kukamilika kwake ili wahusika wafikie hatua ya kufaidika nalo sambamba na upatikanaji wa ruzuku ambalo Wizara ya Afya na Fedha kulisimamia ili kazi za chuo hicho ziende kama zilivyopangwa.

Katika Risala ya wahitimu hao wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya iliyosomwa na Mmoja wa wahitimu hao Rukia Awadhi Suleiman waliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa msimamo wake wa kuimarisha chuo hicho.

Hata hivyo muhitimu Rukia alizitaja baadhi ya changa moto zinazowakumba wanafunzi wa chuo akizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na uhaba wa vifaa vya masomo hasa vitabu katika maktaba yao.

Aidha Rukia alisema ada za wanafunzi pamoja na walimu wao wanaopata elimu ya juu ambao hawarudi kutoa taaluma chuoni hapo ni mambo ambayo yanawapa wakati mgumu kwenye mafunzo yao.

Mapema Mkuu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Dr. Haji Mwita Haji alisema mafunzo ya elimu ya afya yameanza kutolewa hapa Nchini tokea mwaka 1938, Zanzibar ikiweka rikodi ya kuwa miongozi mwa nchi chache barani Afrika kuendesha mafunzo hayo.

Hata hivyo Dr. Mwita alisema mafunzo hayo yalikumbwa na changamoto zilizosababisha wanafunzi wake kuhamia sehemu mbali mbali kutokana na ukosefu wa majengo ya kudumu.

Alisema juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiana na Serikali ya Oman zikasimamia ujenzi wa majengo mapya ya kudumu ya chuo hicho yaliyoanzishwa mwaka 1989 sam,bamba na chuo hicho kuanzishwa rasmi kwa sheria nambari 10 ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Mkuu huyo wa chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya alifafanua kwamba chuo hicho kimepiga hatua kubwa katika ufinyanzi wa wataalamu wa fani ya afya kwa kadi zipatazo nane.

Mahafali hayo ya 21 ya chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya yametoa wahitimu wapatao 280 ambao kati yao Maafisa Tabibu kinga ya Meno wahitimu 13, Afya Tabibu wahitimu 15, Afya Mazingira wahitimu 49 na Uuguzi wahitimu 68.

Wengine ni Utabibu wa Maabara wahitimu 38, Madawa wahitimu 48 wakati Ufundi sanifu wa vifaa vya Hospitali wamehitimu wanafunzi 13.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top