Wizara ya Mifugo na Uvuvi imehimizwa kutoa taaluma zaidi kwa wakulima na wafugaji ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi. 

Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika ziara yake ya kukagua miradi inasimamiwa na Community Forest Pemba kwa kushirikiana na Community Forest International. 

Maalim Seif amesema wakulima na wafugaji bado wanahitaji taaluma ya ziada katika kutekeleza miradi yao, na kwamba Wizara hiyo inajukumu la kuwafikia wajasiriamali hao ili waweze kuongeza ufanisi katika kazi zao. 

Akizungumza na kikundi cha ushirika cha vijiji vya Hindi na Kambini katika Wilaya ya Wete, Maalim Seif amewahimiza wanakikundi hao kuongeza juhudi ili kuhakikisha ushirika wao unaimarika zaida. 

Mapema akisoma risala ya ushirika huo unajishughulisha na ufugaji wa nyuki pamoja na kilimo cha mboga mboga, msaidizi katibu bi. Zuhura Massoud amesema ushirika wao umepata maendeleo makubwa hasa katika kilimo cha mboga mboga. 

Hata hivyo amesema bado wanakabiliwa na tatizo la utaalamu katika ufugaji pamoja na upungufu wa maji katika eneo lao la kilimo, na kuziomba Wizara zinazohusika kusaidia kuwatatulia matatizo hayo. 

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top