Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipongeza Klabu ya Kimataifa ya Rotari ya Mji wa Seattle –Washington Nchini Marekani kwa uamuzi wake iliyochukuwa katika kuunga mkono harakati za maendeleo za Zanzibar hasa katika Sekta ya Elimu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa pongezi hizo katika hafla maalum ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na Klabu hiyo kuwakaribisha Viongozi wapya na kuwaaga wale waliomaliza utumishi wao iliyofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya Red Lion Mjini Seattle Nchini Matrekani.
Balozi Seif alisema ahadi iliyotolewa na Klabu hiyo kwa kuipatia Zanzibar msaada wa Kompyuta kwa ajili ya skuli mbali mbali za Unguja na Pemba umekuwa mkombozi mkubwa ndani ya sekta ya Elimu Nchini.
Alieleza kwamba wanafunzi wa skuli mbali mbali za Msingi kupitiamsaada huo watapata nguvu na uwezo zaidi wa kuweza kukabiliana na masomo yao kwa kutumia mfumo wa kisasa wa Teknolojia ya Habari ulioenea hivi sasa ulimwenguni.
Alisema Klabu za Rotari katika Mataifa mbali mbali duniani zimekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma za Kijamii na maendeleo ya wananchi wao zinazopelekea kubadilisha maisha yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiomba Klabu ya Rotary ya Mji wa Seattle kufikiria mpango maalum wa kutoa mafunzo kwa wananchi wa Zanzibar katika njia na mbinu za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.
Alisema maeneo mengi ya visiwa vya Unguja na Pemba yako katika hali ya hatari kutokana na baadhi ya watu kuchafua mazingira hasa kwenye uchimbaji onvyo wa mchanga samba samba na ukataji kiholela wa misitu bila ya kuzingatia athari zake.
Mapema Rais wa Klabu ya Kimataifa ya Rotary ya Mji wa Seattle Nchini Marekani Bibi Laura Rehrmann alisema Taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1909 imekuwa ikisaidia huduma za kijamii kwa kutoa mafunzo katika Nyanja za Afya na Elimu.
Bibi Laura ameahidi kwamba Klabu yao daima itaendelea kushirikiana na Serikali na Taasisi nyengine sehemu mbali mbali duniani katika kuona huduma za kijamii zinaungwa mkono wakati wote.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake alizitembelea Ofisi za taasisi binafsi inayojishughulisha na utoaji wa huduma na elimu ya afya ya Path katika mataifa mbali mbali duniani iliyopo katika mtaa wa West elm Mjini Seattle.
Katika mazungumzo yao Mkurugenzi wa operesheni ya Kimataifa ya Taasisi hiyo ya Path Adam Silver alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba taasisi yao hivi sasa inatekeleza program tano Nchini Tanzania Bara na Visiwa vya Unguja na Pemba.
Adam Siler alisema akiwaongoza wataalamu kadhaa wa Taasisi hiyo wamekuwa wakitoa huduma za afya katika maradhi ya TB, Ukimwi, udhibiti wa dawa za kulevya pamoja na homa ya Malaria.
Aliushukuru Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar chini ya Katibu Mkuu wake Dr. Saleh Mohammed Jidawi kwa ushirikiano wanaotowa kwa watendaji wa Taasisi hiyo ya Path ambao umewawezesha kutekeleza kazi walizopangiwa kwa mafanikio makubwa.
Naye kwa upande wake Mtaalamu wa maradhi ya T.B Brian Takesin alisema wameshuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana Zanzibar kwa wananchi wengi kuelewa umuhimu wa udhibiti wa maradhi mbali mbali.
“ Yapo mafanikio makubwa katika udhibiti wa maradhi mengi Zanzibar kufuatia muamko wa wakaazi wake mbali mbali “. Alisisitiza Mtaalamu huyo wa Path wa masuala ya TB.
Akitoa shukrani kwa taasisi hiyo kuamua kutoa huduma za Afya Tanzania na Zanzibar kwa ujumla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza watendaji wa Path kwa juhudi zao za kusaidia sekta ya Afya Zanzibar.
Balozi Seif alisema juhudi za Taasisi hiyo hazina budi kuungwa mkono na Taasisi nyengine duniani ili kuona matatizo tafauti ya afya yanayowasumbua Wananchi yanapatiwa ufumbuzi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake amemaliza ziara yake Mjini Seattle – Washington Nchini Marekani na kuondoka leo akitarajiwa kurejea Zanzibar jioni ya Tarehe 18 Novemba kwa kupitia Mjini Dubai.
Atakapowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar anatarajiwa kuzungumza na Waandishi wa vyombo mbali mbali vya Habari nchini kuelezea mafanikio ya ziara yake Nchini Marekani ambapo pamoja na mambo mengine lakini pia alihudhuria mkutano wa 15 wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye asili ya Afrika wa Mji wa Seattle - Washington ya Kaskazini Magharibi ya Pacific.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment