Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imefanikiwa kujenga Skuli mpya za Sekondari 21 ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba kwa nia ya kuimarisha hadhi ya elimu ili iendane sambamba na mabadiliko ya dunia yaliyopo hivi sasa ya sayansi na Teknolojia.
Naibu Katku Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Nd. Abdulla Mzee Abdulla alieleza hayo wakati akitoa ufafanuzi na kujibu maswali kufuatia ushauri na baadhi ya masuala aliyoulizwa na wayajumiya ya Watanzania wanaoishi Katika Mji wa Seattle –Washington Nchini Marekani.
Ndugu Mzee alisema skuli 15 tayari zinaendelea kutoa huduma wakati nyengine sita ziko katika hatua ya kukamilika ili ziweze kutoa huduma kwa wanafunzi wanaoingia ngazi ya sekondari wanaofikia zaidi ya asilimia 64% hivi sasa.
Naibu katibu mkuu huyo wa Wizara ya Elimu Zanzibar aliwaeleza Watanzania hao wanaoishi Marekani kwamba katika kuunga mkono mpango huo wa Serikali Mfuko wa shirika linalosimamia sekta ya mafuta la nchi za Ghuba { Opec } limejitolea kugharamia ujenzi wa baadhi ya Skuli za Msingi Zanzibar.
“ Tuna haki ya kujivunia mafanikio ya sera yetu ya Elimu inayoonekana kutoa matunda mazuri yaliyosaidia kuvuka malengo ya millennia katika sekta ya elimu na kuifanya Zanzibar kuwa katika kiwango cha juu kwenye Mataifa yaliyomo ndani ya Ukanda Jangwa la Sahara Barani Afrika “. Alifafanua Ndugu Abdulla Mzee.
Ndugu Mzee aliwapongeza Watanzania hao wanaoishi Mjini Seattle na Miji mengine Nchini Marekani kwa juhudi zao za kusaidia Sekta ya Elimu Nyumbani Zanzibar na Tanzania kwa jumla na kuwaomba wasichoke waendelee kuunga mkono Sekta hiyo muhimu kwa hatma ya jamii nzima hapo baadaye.
Akizungumzia uimarishaji wa elimu kupitia mfumo wa kisasa wa mtandao wa kompyuta Nd. Abdulla Mzee alieleza kwamba mpango maalum umendaliwa na Wizara kupitia msaada wa Serikali ya Marekani katika kuhakikisha mitaala ya somo hilo kwa hatua ya skuli zote za msingi unguja na pemba inatekelezwa.
Alifahamisha kwamba uhamasishwaji wa wanafunzi wa kike hivi sasa umeongezeka mara dufu katika maskuli mbali mbali ya Zanzibar katika ngazi zote msingi na ile ya Sekondari.
Ndugu Mzee alisisitiza kuwa idadi ya wanafunzi wa kike katika madarasa mbali mbali Nchini imekuwa kubwa ikilinganishwa na ile ya wavulana kiasi kwamba inatoa muelekeo kwa lengo la taifa kutekeleza ile azma yake ya kuweka uwiano wa kijinsia katika maeneo yote ya jamii.
“ Takwimu zinatuonyesha wazi hivi sasa kwamba idadi ya wanafunzi wetu wa kike maskulini iko juu kwa ngazi zote za msingi na ile ya Sekondari”. Aliendelea kufafanua Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Mapema Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi aliwaasa Watanzania hao kuendelea kukumbuka hatma yao ya Nyumbani ambayo ndio itakayokuja wasaidia kuwa na utulivu wa maisha yao ya hapo baadaye.
“ Nyumbani ni Nyumbani tu hata kama mtu ataamua kuendeleza maisha yake nje ya eneo lake la uzawa”. Mama Asha aliwakumbusha Vijana hao kwa kutumia ule msemo maarufu wa Kiswahili usemao Mkataa kwao daima ataendelea kuwa Mtumwa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment