Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema ni jambo la kutia moyo kuona mahusiano na mashirikiano kati ya Oman na Zanzibar yanaendelea kuimarika siku hadi siku.
Amesema mbali na mahusiano ya kiserikali, nchi hizo pia zina uhusiano wa kindugu ambao hauwezi kusahauliwa, hali inayopelekea watu wengi wa Oman kuamua kuja Zanzibar kwa ajili ya mapumziko wakati wa likizo zao.
Akizungumza na Balozi mdogo wa Oman Sheikh Saleh Al-Hafidh, aliyefika Ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi, Maalim Seif amesema mahusiano hayo yatazidi kuimarishwa kwa maslahi ya pande zote mbili.
Amesifu kazi nzuri iliyofanywa na balozi huyo katika kipindi kifupi cha miezi mitatu alichofanya kazi Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kuratibu na kufanikisha kufanyika kwa Tamasha la Kiislamu hapa nchini.
Amemtaka Sheikh Saleh aendelee kuwa balozi wa kuitangaza Zanzibar nchini Oman na nchi nyengine atakazokwenda kuzifanyia kazi.
Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais amesifu juhudi zinazochukuliwa na Sultan Qaboos wa Oman katika kuisadia Zanzibar katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi na kitaaluma.
Amesema mara zote Sultan Qaboos amekuwa akitekeleza ahadi zake za kuisaidia Zanzibar, na kuonyesha mashirikiano makubwa katika kuwaendeleza Wazanzibari kupata elimu ya juu ambapo tayari ametoa nafasi kadhaa za masomo nchini Oman.
Kwa upande wake Balozi mdogo wa Oman Sheikh Saleh Al-Hafidh, ameishukuru Serikali na wananchi wa Zanzibar kwa kumpa mashirikiano mazuri yaliyorahisisha kutekeleza majukumu yake ya kikazi kwa ufanisi.
Amesema ataendelea kushirkiana na Zanzibar wakati wowote licha ya kumaliza muda wake wa utumishi hapa nchini, na kwamba amepata moyo huo baada ya kujionea mwenyewe ukarimu na ustaarabu wa Wazanzibari ambao kwa kiasi kikubwa unashabihiana na ule wa watu wa Oman.
Hassan Hamad (OMKR)
0 comments:
Post a Comment