Chama Cha Wananchi (CUF) kimesema kinaisubiri kwa hamu rasimu ya pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili kuona ikiwa maoni yao yamezingatiwa au laa.

Akizungumza na wafuasi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Muwanda Donge, Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amesema miongoni mwa madai yao ni pamoja na kuainishwa mipaka ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.

Kuhusu Bunge la Katiba Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amewashauri wajumbe wa Zanzibar watakaoingia kwenye Bunge hilo kuungana na kuzingatia maslahi ya Zanzibar badala ya kushikilia misimamo ya vyama.

Amefahamisha kuwa ikiwa Wazanzibari wataungana katika kutetea maslahi ya nchi yao, Zanzibar itaweza kujikomboa na kupiga hatua kubwa za maendeleo katika kipindi kifupi kijacho.

Aidha amesema Chama chake kitaendelea na msimamo wake wa kudai mamlaka kamili ya Zanzibar hadi hapo yatakapopatikana, na kwamba awamu zote za uongozi zilizopita Zanzibar zimekuwa zikipigania haki hiyo kwa maneno tofauti.

Amelipongeza jeshi la polisi kwa kushirikiana na chama hicho katika kufanikisha mkutano huo ambao mara zote ulishindwa kufanyika katika eneo hilo.



Hassan Hamad (OMKR)

0 comments:

 
Top