Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anaondoka Nchini leo jioni kuelekea Washington kuhudhuria Mkutano wa 15 wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye asili ya Afrika ya Kaskazini Magharibi mwa Picific unaotarajiwa kufanyika katika Jimbo la Seattle Nchini Marekani.

Balozi Seif amepata heshima hiyo kufuatia ujumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye asili ya Afrika kutoka Marekani uliowahi kufanya ziara hapa Zanzibar kati kati ya mwezi wa April Mwaka huu na kujionea mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo Zanzibar imepatiwa fursa ya kwenda kujitangaza Nchini humo.

Mtandao wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye asili ya Afrika Nchini Marekani umeamua kufungua ukurasa mpya katika kuona inaendeleza mashirikiano na Nchi rafiki ikilenga kusaidia taaluma na hata uwezeshaji kwa Taasisi na Mashirika Barani Afrika ili yajinyanyue kiuchumi.

Katika ziara hiyo ya wiki moja ya Kiserikali itakayotoa pia fursa ya kutembelea baadhi ya Makampuni na Taasisi za Umma, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar anauongoza ujumbe wa Viongozi saba wa Serikaliwakiwamo Mawaziri, Watendaji wa serikali na Maafisa waandamizi.

Viongozi anaofuatana nao ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed, Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Mh. Nassor Ahmed Mazrui pamoja na Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Mh. Hamza Hassan Juma.

Wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha wafanyabiashara Zanzibar Abdulla Abass, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Ali Khalil Mirza, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Abdulla Mzee Abdulla,Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bahari Kuu Zahor Mohammed El- Kharousy pamoja na timu ya wafanyabiashara wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake akiambatana na baadhi ya wafanyabaiashara maarufu hapa Zanzibar atapata fursa ya kutembelea Kampuni ya utengenezaji wa ndege za Abiria na mizigo ya Baeing Mjini Seattle, kukutana na Uongozi wa Mfuko wa misaada wa Melinda Gates na ule wa Microsoft pamoja na jumuiya ndogo ndogo za wafanyabiashara.

Maeneo mengine watakayopata fursa ya kutembelea ni ni baadhi ya Taasisi za Serikali, Meya wa Jiji la Seattle ziara iakayoambatana pia na vikao na Mikutano ya Wafanyabiashara wa Zanzibar na Mji huo katika kubadilishana mawazo na kuanza kupanga mikakati ya ushirikiano.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amepanga kukutana na Wanachama wa Jumuiya ya Wazanzibari na Watanzania wanaoishi Mjini Seattle na Washington kwenye Tafrija maalum waliyojipanga kumuandalia yeye na ujumbe wake aliofuatana nao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif anatarajiwa kukamilisha ziara yake Mjini Seattle Nchini Marekani Mnamo Tarehe 14 Novemba 2013 na kurejea nyumbani kwa kupitia Dubai.

Mapema asubuhi kabla ya kuondoka Nchini kuelekea Marekani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Balozi Mdogo mpya wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Bwana Xie Yunliang ambae alifika kujitambuluisha rasmi.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar Viongozi hao walielezea haja ya pande hizo mbili kuendelea kushirikiana katika miradi ya maendeleo China ikiwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika uimarishaji uchumi na ustawi wa Jamii.

Balozi Xie Yungliang alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba China itaendelea kuunga mkono harakati z maendeleo za Zanzibar katika kujiletea maendeleo na kupunguza umaskini.

Alisema China ilitenga zaidi ya Yuan Milioni Mia moja katika kuunga mkono miradi ya Skuli, awamu ya Pili ya ujenzi wa uwanja wa ndege bwa Kimataifa wa Zanzibar Kisauni pamoja na ile awamu ya Pili ya mradi wa Mkongo wa Mawasiliano hapa Zanzibar.

Naye akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza Jamuhuri ya Watu wa China kwa jitihada zake za makusudi za kuona Zanzibar inajikwamua kutoka katika wimbi la umaskini.

Balozi Seif alimuahidi Balozi huyo Mdogo mpya wa Jamuhuri ya Watu wa China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kumpa ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa majuku yake aliyopamngiwa na Nchi yake.

Baadaye Balozi Seif pia alifanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Oman hapa Zanzibar Bwana Saleh Suleiman Al - Harith ambae naye alifika kujitambulisha bada ya kuteuliwa na Nchi yake kufanya kazi ya Kidiplomasia hapa Zanzibar.

Mazungumzo yao yalijikita zaidi katika kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Nchi hizo ambao ni wa kihistoria kutokana na maingiliano ya kidamu ya wananchi wa pande hizo mbili.

Balozi Seif alimueleza Balozi Mdogo wa Oman Nchini kwamba Zanzibar Zanzibar inahitaji kuwa na viwanda vidogo vidogo hasa vya matunda ilikuweza kusaidia uchumi wake.

Alisema wananchi wengi hasa wakulima wamekuwa wakizalisha idadi kubwa ya matunda ambayo baadaye hupotea na kuleta hasara kutokana na wakulima hao kukosa utaalamu wa hifadhi ya matunda hayo.

Aliipongeza Oman kwa misaada yake mikubnwa inayoendelea kutoa kwa Zanzibar katika Nyanja za za maendeleo ambayo inazidi kuimarisha uhusiano uliopo kati ya mataifa hayo mawili.

Naye kwa aupande wake Balozi mdogo wa Oman hapa Zanzibar Bwana Saleh Suleiman Al –Harith amewapongeza Viongozi na Wananchi wa Zanzibar kwa ushirikiano waliompa uliomuwezesha kutekeleza majukumu yake vizuri katika kipindi kifupi cha utumishi wake.

Balozi Saleh alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba lile ombi la Zanzibar la kutaka mkutano wa ushirikiano wa wafanyabiashara wa Nchi za Ghuba Oman ikiwa mratibu atalifikisha katika ngazi zinazohusika wakati ataporejea Nchini mwake.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top