Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alisema Viongozi na Wanachama wa CCM wanapaswa kuendelea kufanya vikao vyao kwa mujibu wa Kanuni na Taratibu za Chama hicho ili kuwa na uhalali kamili wa maamuzi wanayoyatoa kuhusu chama chao.

Kauli hiyo aliitoa wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Tawi la Chama cha Mapinduzi la Kijiji cha Kiomba Mvua na baadaye kukabidhi vifaa mbali mbali vya uendelezaji ujenzi wa Tawi hilo.

Vifaa alivyokabidhi Balozi Seif ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mbunge wa Jimbo la Kitope ni pamoja na Mabati, saruji, mchanga kokoto, nondo, mbao pamoja miti kwa ajili ya ukamilishaji wa Tawi jipya la Kijiji hicho.

Hafla hiyo ilikwenda sambamba na Vikundi vya Polisi jamii vya Kijiji cha Kitope na Mbaleni kukabidhiwa Fedha taslimu na ahadi za fulana kwa ajili ya kuimarisha kazi za za ulinzi, mchango na vifaa vyote hivyo vikigharimu jumla ya Shilingi Milioni 4,000,000/-

Balozi Seif alisema maamuzi ya chama kwa mujibu wa kanuni za CCM hutakiwa kufanyika ndani ya vikao halali vya Viongozi na wanachama wenyewe jambo ambalo husaidia kuepusha minong’ono na hata majungu miongoni mwa wanachama wa chama hicho.

Alitahadharisha kwamba maamuzi ya chama hayatolewi bara barani na ndio maana Katiba ya CCM ikasisitiza kujengwa Ofisi bora za chama hicho na zenye kwenda na wakati zinazolingana na hadhi ya chama ili wana chama hao wapate fursa nzuri ya kutoa maamuzi kwenye ofisi zao.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi aliwapongeza wana CCM wa Tawi hilo kwa uamuzi wao wa kujenga Tawi Jipya na la Kisasa likiwa pia na sehemu ya miradi ya kiuchumi.

“ Chama cha Mapinduzi katika ngazi zake zote lazima kiwe na miradi ya kiuchumi itakayosaidia utekelezaji wa kazi za chama hicho katika ngazi husika ili kujilinda na utegemezi kutoka ngazi za juu za chama “. Alisisitiza Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba uwamuzi wao huo ni sahihi na unakwenda sambamba na lengo la Chama ndani ya Jimbo la Kitope la kuwa na Ofisi mpya za kisasa zinazokwenda na wakati

Alieleza faraja yake kuona kwamba Jimbo la Kitope katika Matawi yake 20 hadi sasa tayari Ofisi 16 za chama cha Mapinduzi zimeshakamilika kujengwa majengo mapya ikibakisha Matawi manne tu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top