Kikao cha Kamati ya Taifa ya Maadhimisho ya sherehe na Mapambo Zanzibar kimekutana kutathmini maadhimisho ya Sherehe zilizopita za Kutimia miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 yaliyowakomboa Wakwezi na Wakulima wa Taifa hili.

Wajumbe wa Kikao hicho wakiwa chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wamekutana katika ukumbi wa nyuma wa Jumba la Wananchi Forodhani Mjini Zanzibar.

Akiwasilisha Taarifa ya Tathmini hiyo Kaimu Katibu wa Sekriterieti ya Kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Said Shaaban alisema kwamba Kamati zote zimetekeleza vyema majukumu yake kama zilivyopangiwa.

Nd. Said aliwaeleza wajumbe hao kuwa licha ya ufanisi huo lakini zipo baadhi ya changamoto zilizojichomoza ndani ya utekelezaji wa kamati hizo ambazo alizitaja kuwa ni ufinyu wa Bajeti kulingana na shughuli zilivyopangwa pamoja na ushiriki mdogo wa maafisa wa Serikali na Masheha kwa dhana ya kwamba wao sio wahusika.

Nd. Said alisema katika kufanikisha nusu karne ya Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 50 Sekriterieti imependekeza kutumiwa vyema vyombo vya Habari hasa vile vya Serikali katika kushajiisha umma kuelewa umuhimu wao wa kushiriki vyema katika maadhimisho hayo ya kihistoria.

Akitoa nasaha zake Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Taifa ya Maadhimisho ya Sherehe na Mapambo ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alizipongeza kamati zote kwa kufanikisha vyema sherehe za kutimia miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Balozi Seif alifahamisha kwamba sherehe za miaka 49 zimefanikiwa vyema kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Viongozi, Wafanyakazi wa Taasisi za Umma na zile binafsi pamoja na Wananchi.

“ Wajumbe wakati tunaipokea Tathmini hii ya sherehe za maadhimisho ya kutimia miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar tunapaswa kuanza safari kubwa ya sherehe hizi kutimia miaka 50 ya Mapinduzi yetu matukufu sawa na kusema Nusu Karne”. Alieleza Balozi Seif.

Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Maadhimisho ya Sherehe na Mapambo wanatarajiwa kukutana tena katika kipindi cha mwezi mmoja ujao kuendelea kupanga mikakati ya maandalizi ya maadhimishop hayo ya Nusu Karne ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akakiongoza Kikao cha Kamati ya Maafa Zanzibar kujadili namna ya Taifa linavyoweza kujiandaa dhidi ya maafa au matatizo yoyote yanayoweza kutokea katika kipindi hichi cha mvua za masika zilizokwishaanza.

Kikao hicho kilichojumuisha wajumbe wa kamati hiyo kutoka Unguja na Pemba kilifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyopo Vuga Mjini Zanzibar.

Akiwasilisha Taarifa juu ya mwelekeo wa Mvua za Masika mwezi wa Machi hadi Mei mwaka huu Mkurugenzi wa Idaya ya Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad alisema pamoja na kuwa na matarajio ya mvua za wastani katika maeneo mengi, lakini bado upo uwezekano wa kutokea miripuko ya magonjwa.

Ndugu Hamad alisema taasisi zinazohusika na maafa zinapaswa kuchukuwa hatua za tahadhari katika maandalizi ya kukabiliana na madhara yanayoweza kusababishwa na Mvua za masika za mwaka huu.

Akizungumzia sekta ya kilimo na usalama wa chakula Nd. Hamad alisema maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini pamoja na Visiwa vya Zanzibar yanatarajiwa kuwa na unyevu unyevu wa kutosha wa udongo hali ambayo wakulima wanashauriwa kuendelea na taratibu za kawaida za Kilimo cha msimu wa mvua za masika.

Akikiahirisha Kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Maafa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliiagiza Idara ya Maafa Zanzibar kwa kushirikiana na wataalamu wa Taasisi washirika kuandaa utaratibu mahsusi wa kutoa taarifa rasmi kwa Wananchi mapema wiki ijayo itakayosaidia Jamii kuwa na hadhari dhidi ya majanga yoyote yanayoweza kutokea katika mvua za masika.

Balozi Seif alisema Serikali pamoja na Jamii yote inapaswa kujitayarisha na hali yoyote ya majanga au maafa kulingana na msimu wa masika uliokwishaanza mapema mwezi huu.

Wakichangia katika Kikao hicho baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo wamesema Wananchi walio wengi hadi sasa hawajawa na utamaduni ya kufuatilia mienendo ya mifumo ya hali ya hewa nchini ambayo ni muhimu katika maisha yao ya kila siku. 
 
Othman Khamis Ame  
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top